Shirika la Habari la Hawza | Kuhusu udharura wa kuwepo kwa Imam, hoja nyingi zimetolewa, lakini sisi tutatosheka na maelezo rahisi tu:
Hoja ile ile inayothibitisha haja ya kuwepo kwa Mtume, pia inaonyesha haja ya watu kuwa na "Imam"; kwa sababu kwa upande mmoja, uislamu ni dini ya mwisho na Mtume Muhammad – rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake – ni Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, hivyo basi uislamu lazima uweze kujibu mahitaji yote ya mwanadamu hadi Siku ya Kiyama.
Kwa upande mwingine, Qur’ani tukufu imeeleza misingi na jumla ya hukumu na maarifa ya kimungu, na maelezo na ufafanuzi wake umeachiwa Mtume – rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake. [1]
Hata hivyo, ni wazi kuwa Mtume – rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake – akiwa kama kiongozi wa Waislamu, alifafanua aya za Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa mahitaji na uwezo wa jamii ya kiislamu ya wakati wake. Hivyo, ni lazima awepo mrithi wake aliye na sifa stahiki ambaye kama yeye, ana uhusiano wa moja kwa moja na bahari isiyo na mwisho ya elimu ya Mwenyezi Mungu, ili afafanue yale ambayo Mtume – rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake – hakuyabainisha na ajibu mahitaji ya jamii ya kiislamu katika kila zama.
Katika riwaya iliyopokewa na Mashia na Masunni kutoka kwa Mtume – rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake – imesemwa:
«اِنّی تارِکٌ فیکُمُ الثَّقَلَینِ کِتابَ اللّهِ وَ عِتْرَتی؛ ما اِنْ تَمَسَّکْتُمْ بِهِما لَنْ تَضِلّوُا بَعْدی اَبَداً.»
"Hakika mimi nimewaachia vizito viwili: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu (Ahlul Bayt wangu); kama mtashikamana navyo basi kamwe hamtapotea baada yangu milele." [2]
Kwa mujibu wa hadithi hii, uwepo wa kizazi cha Mtume sambamba na Qur’ani ni jambo la lazima.
Vilevile, Maimamu – amani iwe juu yao – ni walinzi wa mirathi ya Mtume – rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake – na wao ndio wanaotoa maelezo sahihi na wafasiri wa kweli wa Qur’ani tukufu, ili dini ya Mwenyezi Mungu isije ikaharibiwa na wenye chuki au maadui, na chemchemi hii safi iendelee kuwa safi na salama hadi siku ya kiyama.
Zaidi ya hayo, “Imamu” akiwa kama mwanadamu kamili, ni mfano wa kipekee na kamili katika nyanja zote za kibinadamu. Na mwanadamu ana haja ya dharura ya kuwa na mfano kama huu, ili kwa msaada na uongofu wake, apate kulelewa kwa namna inayostahiki ukamilifu wa kibinadamu, na kwa mwangaza wa maelekezo ya mlezi huyu wa mbinguni, ahifadhiwe dhidi ya upotofu na kufanya maasi nafsi na mashetani wa nje.
Imamu Swadiq – amani iwe juu yake – amesema kuhusu jambo hili:
«إِنَّ اَلْأَرْضَ لاَ تَخْلُو إِلاَّ وَ فِیهَا إِمَامٌ کَیْمَا إِنْ زَادَ اَلْمُؤْمِنُونَ شَیْئاً رَدَّهُمْ وَ إِنْ نَقَصُوا شَیْئاً أَتَمَّهُ لَهُمْ.»
"Hakika ardhi haibaki bila ya Imam; ili kama waumini wakiongeza jambo [katika dini], awarejeshe, na wakipunguza jambo, alitimilizie." [3]
Kutokana na maelezo ya hapo juu, imekuwa dhahiri kuwa haja ya watu kwa Imam ni haja ya kimsingi, na baadhi ya majukumu ya Imam ni haya yafuatayo:
- Kuongoza na kusimamia mambo ya jamii (kuunda serikali)
- Kulinda dini na mila ya Mtume dhidi ya upotoshaji na kutoa tafsiri sahihi ya Qur’ani
- Kusafisha nafsi na kuwaongoza watu kiroho [4]
Utafiti huu unaendelea…
Rejea:
1. Qur’ani Tukufu inamwambia Mtume wa Uislamu – rehma na amani ziwe juu yake na Aali zake: “Na tumekuteremshia wewe Ukumbusho [Qur’ani] ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao.” (Surat An-Nahl, aya ya 44)
2. Bihar al-Anwar, juzuu ya 2, ukurasa wa 100
3. Al-Kāfi, juzuu ya 1, ukurasa wa 178.
4. Inafaa kusemwa kuwa “kuunda serikali” kwa upande wa Imam Maasumu kunategemea mazingira na masharti maalumu, lakini majukumu mengine yanatekelezwa hata katika kipindi cha ghaiba, ingawa wakati wa kudhihiri kwa Imam na kuwepo kwake waziwazi miongoni mwa watu, majukumu hayo yanakuwa dhahiri na yenye kushikika. Jambo jingine ni kuwa yale yaliyosemwa katika sehemu hii yanahusu haja ya watu kwa Imam katika maisha yao ya kiroho, lakini haja ya ulimwengu mzima kwa “uwepo wa Imam” itajadiliwa katika mada ya “Faida za Imam aliyeughaibuni.” inshaAllah.
Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho "Negine Afarinesh", likini kuna mabadiliko kiasi.
Maoni yako